CUF yawashutumu mjumbe wa Tume ya Warioba, mwakilishi wa CCM kuharibu Maoni

Zanzibar Daima imeipokea taarifa ifuatayo ambayo imetolewa na Kurugenzi ya Uenezi ya Chama cha Wananchi (CUF) kwa vyombo vya habari. Hapa tunaishapisha kama ilivyo kwa manufaa ya mjadala wa umma.

“Bila shaka Mchakato wa Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umekuwa ukiendelea nchini kote kwa mujibu wa sheria na pia kuitekeleza haki ya msingi ya wananchi kushiriki na kuwasilisha maoni yao ambayo ni sehemu muhimu ya maamuzi yatakayoamua hatma ya nchi kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

 

“Kwa upande wa Zanzibar, na kama ilivyo nchini kote, zoezi la wananchi kutoa maoni juu ya Katiba waitakayo linaelekea ukingoni, likiwajumuisha wananchi wa Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, walioonekana kujitokeza kwa wingi, mbele ya Tume ya Kuratibu Maoni, nao wakitekeleza haki yao ya kidemokrasia.

 

“Kwa Wilaya ya Mjini Unguja, zoezi hilo limekuja wakati muafaka ambapo Ulimwengu unaadhimisha miaka 64 ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Binaadamu, iliyotokana na Azimio la Umoja wa Mataifa la Disemba 1948 ambalo Tanzania, Zanzibar ikiwa sehemu yake, ni mwanachama wake; na kwamba matarajio ya umma na eerikali kwa ujumla yalikuwa ni kushuhudia “sauti” ya wananchi ikisikika kama ilivyo kauli ya mwaka huu ya Umoja wa Mataifa kwamba “SAUTI YANGU NI MUHIMU” yaani ‘MY VOICE COUNTS’.


“La kusikitisha mno, ambalo ni kinyume na Sheria na pia linalokiuka maagizo hata ya Viongozi Wakuu wa Nchi hii, akiwamo Raisi wa Jamhuiri ya Muungano wa Tanzania Mhe Jakaya Kikwete, na pia Raisi wa Zanzibar, Mhe Dokta Ali Mohamed Shein, ya kuwataka wananchi wapewe uhuru wa kutoa maoni yao, ni kuona kwa makusudi wananchi wa Zanzibar wakinyimwa HAKI YAO YA KUTOA MAONI, mbele ya Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni juu ya Marekebisho ya Katiba.


“Hilo limetendeka Mchana wa Jumatatu hii, tarehe 10 Disemba, 2012, katika Kiwanja cha Mzalendo, Jimbo la Magomeni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, kutokana na kile kilichothibitika kuwa ni hila na ushawishi wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambaye ni Muwakilishi wa Jimbo hilo, Bw. Salmin Awadh Salmin, pamoja na Waziri Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi Fatma Said Ali, ambaye pia ni Kamishna wa Tume hiyo, waliolivuruga zoezi hilo na hatimaye Wananchi kushindwa kabisa kutoa maoni yao.


“Chama cha Wananchi, CUF, kimeshtushwa sana na hali hiyo ambayo wazi wazi imelenga kuchafua zoezi halali, na pia kuinyima Mamlaka halali (Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba) nafasi yake ya kuendesha harakati zake, usoni kwa umma, kutokana na jeuri ya kisiasa na utashi binafsi.


“Masikitiko makubwa ni kwamba, tokea Zoezi hilo lilipoanza katika Mkoa wa Kusini Unguja, mnamo tarehe 2 Julai, 2012, na hadi tarehe 5 Disemba, 2012 lilipomaliza katika Wilaya ya Magharibi Unguja, haijawahi kutokea hali hiyo wala kile kinachochukuliwa na Umma wa Wananchi wa Zanzibar, kuwa ni kitendo cha jeuri na ufedhuli, usioweza kuvumilika.


“Pamoja na busara nyingi zilizotumika kuepusha maafa, na kuitaka Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba pia kuwaomba radhi wananchi ambao walikwishahudhuria Kituoni hapo, kwa ajili ya kuwasilisha maoni yao, Chama cha CUF kinatoa wito kwa mamlaka husika kuwachukulia hatua za kinidhamu Viongozi sasa ni wakati wa Tume kuchukua hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria ili kuondoa jeuri na kiburi vya viongozi madhalimu hao ambao watapeleka kuvuruga zoezi hilo muhimu katika nchi yetu.


“Chama cha Wananchi, CUF, pia kinaiarifu na kuitanabahisha Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba, kuwa Umma wa Wananchi wa Zanzibar sasa umekosa imani na baadhi ya Makimishna wa Tume hiyo, akiwamo Bi Fatma Said Ali, kwa kushindwa kuficha hisia na ukereketwa wa kisiasa.


“Chama cha CUF, kinauarifu umma na pia kuikumbusha Tume ya Kuratibu Maoni ya Wananchi kwamba walichotenda Viongozi hao ni uvunjifu wa amani, kinyume na Sheria na pia kukiuka Kifungu cha 21 (a) (i)(ii) na kama ambavyo adhabu yake imetajwa katika Kifungu C cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.”

SALUM BIMANI
MKURUGENZI HAKI ZA BINAADAMU, HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA – CUF
HAKI SAWA KWA WOTE

3 thoughts on “CUF yawashutumu mjumbe wa Tume ya Warioba, mwakilishi wa CCM kuharibu Maoni

  1. Weona mambo hayendi watakavo. Bado wana ishi kwenye ndoto ya ulimengu wa kiza wa wewallah bwana. Dunianiani kweupe sasa wana adamu wote wadai haki zao.
    TUNATAKA NCHI YETU SASA TUMECHOKA!

  2. Mimi sielewi knnwiai hata kwa suala hili la ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba iliyopo sasa(ya zamani)na mapendekezo ya katiba mpya,bado kuna ukakasi na kigugumizi kwa sana katika mchakato mzima na utaratibu unaotumiwa na Tume ya Kukusanya Maoni.Utaratibu unaotumika kwa maoni yangu,”kwa kweli umepitwa na wakati,na si dhani kama utazaa matunda yaliyokusudiwa”.Wigo wa utoaji maoni upanuliwe zaidi.Tume iweke wazi anuani zao za mitandao,email addresses,ambazo watanzania popote pale watakuwa huru kutoa na kuwasilisha maoni na mapendekezo yao.Tume ya Katiba,wajaribu kuwa na vipindi vya majadiliano ya wazi kupitia Televisheni mbalimbali hapa nchini,wao watatoa ufafanuzi kama watoa mada,kisha wasikilizaji na watazamaji wawe huru kutoa maoni yao na mapendekezo yao.Zote hizo ziwe nyenzo mbalimbali za kupokea maoni kutoka kwa watanzania wote.Pia,watanzania wawe huru kuandika makala mbalimbali kuhusu mapendekezo ya Katiba Mpya.Nayo hayo yachukuliwe katika kumbukumbu za Tume kama ni michango halali ya watanzania kuhusu muundo wa Katiba Mpya.Mashuleni na Vyuoni,walimu nao wachukue nafasi zao,kwa kuwa na vipindi au madarasa maaluum ambayo yatawezesha wanafunzi na wanazuoni,kuchangia mawazo kwa kutoa mawazo mapya na mapendekezo mapya,ambayo,yataweza kurekodiwa na picha zikapigwa,na kumbukumbu zake zikawasilishwa kwa Tume ya Katiba Mpya.Na mikakati mingine mingi ya aina hiyo.Tukumbuke kwamba,katika zoezi hili,MUDA SI RAFIKI YETU!Kitu cha muhimu kwa Tume,sio kuona Sura za watu au wachangiaji ndipo wazinukuu,ni muhimu lakini siyo LAZIMA!Kitu cha Lazima hapa ni MAWAZO,MAONI,MAPENDEKEZO,na Ushauri,kuhusu kwanza,Mapungufu na Mikanganyiko iliyoko kwenye Katiba ya sasa,na knnwiai,sasa itolewe,NA ni mapendekezo gani ambayo watanzania (kila mchangiaji kwa nafasi yake)wangependa kuona yakijumuishwa katika Katiba Mpya!Na pia Tume ingekuwa na utaratibu wa kuwatangazia wote,kwamba,eneo lolote lile la Tanzania ambalo halijafikiwa na Tume,na wao wanaona wangependa kukutana na Tume hiyo,basi watoe taarifa mara moja,kupitia kwa vyombo vya habari au mwakilishi wao watakaye mpa jukumu hilo.Ili kila sehemu iridhike kwamba imeshirkishwa kikamilifu katika zoezi hilo.Tume iitikie mialiko kwenda sehemu yoyote ya nchi ambako itahitajika kwenda,iwapo bado Tume haifika katika maeneo hayo.Lakini,sio sahihi kwa Tume kupanga Ratiba yake kwa jinsi itakavyoona au itakavyo jisikia.Hili sio jukumu la Tume kuamua.Ni jukumu la “Wenye Katiba Yao(watanzania wenyewe pale walipo)kuamua na kuridhika kwamba wameshirikishwa na maoni yao yamezingatiwa.Sasa hivi kwa jinsi nionavyo mimi,sina hakika iwapo,Tume ya Katiba,inahesabu michango ya mawazo kuhusu Katiba Mpya kupitia magazetini,midahalo ya vyuoni,mikutano ya hadhara,vipindi vya majadiliano katika televisheni mbalimbali,maoni kupitia mitandao,na kadhalika,”kama ni nyaraka halali na muhimu katika kazi yao ya kukusanya maoni na mapendekezo kuhusu Katiba Mpya”.Ni ushauri wa bure tu!Mimi mwenyewe sijaridhishwa na jinsi zoezi zima linavyo endeshwa.Suala muhimu hapa ,ni mawazo,maoni na mapendekezo.Siyo kuona sura za watu wanaochangia,ni muhimu lakini siyo lazima kama fursa hiyo haipo.Mawazo yatakayo faa ndiyo yatakayo zingatiwa,ya kipuuzi yatapuuzwa!Nawapongeza sana Jukwaa La Katiba na Mwenyekiti Deus Kibamba,kwa kazi kubwa na nzuri manyofanya na mliokwisha kuifanya hadi sasa!Mungu awazidishie ujasiri,busara na mwangaza zaidi!

  3. MasalaKulangwa, Kwanza nakupa pole kwa kupoteza muda wako ukikokotoa yale yasemwayo na wanasiasa wa Tanzania. Ila tu ninakushauri, kama utaendelea kukokotoa kauli zao, tafuta kwanza vidonge vya kuzuia shinikizo la damu au mtembelee kwanza daktari.Tanzania yetu Kwa sasa haina siasa safi, na siasa safi inapatikana tu pale nchi inapokuwa na viongozi bora.  Kwa hiyo, hata kauli na matamshi ya 'wanasiasa' wetu yanakuwa ya hovyo hovyo.Ubinafsi wa kiwango cha juu ndiyo umesababisha/unasababisha kutokuwa na siasa safi na uongozi bora na tusishangae pale tunapokuwa na viongozi wa aina hii kwa sababu tumeruhusu wawepo.'Viongozi wetu wa kisiasa' ukiwaangalia kwa nje wanavutia kwelikweli. Wamejawa maneno matamu lakini ukiyakokotoa utagundua niya kibinafsi, binafsi.These so called Tanzanian politician,  they treat us with contempt and We have became their politics punching bagAma kweli, Jamii hovyo hovyo inazaa viongozi hovyo hovyo

    http://www.findlifequotesonline.com/ http://www.findinsurrates.com/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You may use these HTML tags and attributes: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <strike> <strong>